Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia Jonas Mushi, mkazi wa Manushi wilayani Moshi, kwa tuhuma za kumuua Baba yake mkubwa pamoja na mke wa Baba yake mkubwa kwa kuwacharanga na panga, kisa kikidaiwa kuwa ni imani za kishirikina.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema Julai 19 mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika kijiji cha Manushi kati, mtuhumiwa alifika nyumbani kwa marehemu na kuingia ndani na kuchukua panga na kuanza kumshambulia baba yake mkubwa aitwae Mariki Mushi.
Amesema wakati mtuhumiwa akiendelea kumshambulia baba yake mkubwa, mke wa marehemu Felister Mushi aliingilia kwa lengo la kumsaidia mume wake, na ndipo mtuhumiwa akaanza kumshambulia mama yake mkubwa.
Kwa muujibu wa Kamanda Maigwa, mtuhumiwa aliwashambulia kwa kuwakatakata na panga sehemu mbalimbali za miili yao mpaka alipohakikisha wote wamefariki dunia.
Jonas alikuwa akiwatuhumu marehemu kuwa ni wachawi na wamekuwa wakimroga.
Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospitali ya mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi.