NARCO kuanza ununuzi wa mifugo

0
154

Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) imepanga kuanza operesheni maalum ya ununuzi wa mifugo kwa wafugaji kwa bei elekezi, lengo likiwa ni kuboresha sekta ya mifugo nchini.

Akizungumza baada ya kujionea hali ya mifugo katika ranchi ya Taifa ya Kalambo mkoani Rukwa, Mwenyekiti wa bodi ya NARCO Mhandisi Cyprian Luhemeja ameiagiza menejimenti ya kampuni hiyo kuwasilisha bei elekezi kwa kilo moja ya ng’ombe hai, ili iweze kupitiwa na kuidhinishwa na hatimaye zoezi la ununuzi mifugo lianze.

Amesema hatua hiyo itaiwezesha NARCO kuwa na idadi kubwa ya mifugo, itakayoweza kunenepeshwa na kuuzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi ikiwemo nchi jirani za Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambazo zina uhitaji mkubwa wa nyama.

Aidha Mhandisi Luhemeja amesema, hatua hiyo itawawezesha wafugaji kupata soko la uhakika la mifugo yao na kuepukana na wachuuzi ambao wamekuwa wakiwanyonya kwa kupanga bei ndogo, na wafugaji kuendelea kuishi katika umaskini.

Ameongeza kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza migogoro ya wafugaji na wakulima hasa kipindi cha kiangazi na vilevile kuharibu vyanzo vya maji.

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan alimteua Mhandisi Cyprian Luhemeja kuwa Mwenyekiti wa bodi ya NARCO na kuitaka kampuni ya Ranchi za Taifa kutekeleza majukumu yake katika ubora unaotakiwa.