Kampuni 19 zimejitokeza kuwekeza kwenye usambazaji wa gesi asilia inayotumika kuendeshea magari nchini.
Kampuni hizo zimejitokeza kufuatia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kutangaza fursa hiyo ya uwekezaji kwa wazawa.
Kauli hiyo imetolewa mkoani Dar es Salaam na Mhandisi Dora Ernest kutoka TPDC, wakati wa mahojiano kwenye kipindi Cha Jambo Tanzania kinachorushwa hewani na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Amesema TPDC imejipanga kusambaza kwa kasi nishati hiyo ambayo imekuwa na bei nafuu kwa watumiaji kuliko mafuta.
Kwa mujibu wa Mhandisi Dora, kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023, TPDC imejipanga kujenga vituo vinne vya mfumo wa CNG ambapo kituo kimoja kitakuwa kituo mama kitakachojengwa mkoani Dar es Salaam ambacho kitatumika kujaza gesi kwenye magari.
Vituo vingine vitatu vidogo vitajengwa maeneo ya hospitali ya Taifa Muhimbili na soko kuu la samaki feri mkoani Dar es Salaam na pia katika eneo la viwanda Zegeleni, Kibaha mkoani Pwani katika kiwanda cha dawa cha Kairuki.
Kwa upande wake Afisa Habari wa TPDC Marie Msellem amesema, shirika hilo linasimamia miradi ya kimkakati ya kitaifa mitano likiwemo bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda kwenda Tanga – Tanzania, utafiti wa mafuta katika bonde la Eyasi Wembere, mradi wa gesi asilia Mnazi Bay na mradi wa gesi asilia Songosongo.
Amesema gesi asilia inayozalishwa TPDC ni ya gharama nafuu ikilinganishwa na nishati nyingine
ambapo gesi ya shilingi elfu moja inaweza kupika chakula cha watu sita kwa siku.