Homa ya Mgunda yagundulika Ruangwa

0
200

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema, upimaji wa sampuli za wagonjwa waliokuwa wakiugua ugonjwa usiojulikana katika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi umethibitisha ugonjwa huo ni Leptospirosis Field Fever, kwa kiswahili homa ya Mgunda.

Waziri Ummy amesema hayo mara baada ya kutembelea wilaya ya Ruangwa, ambako kumezuka mlipuko wa ugonjwa huo.

Amesema homa ya Mgunda ni miongoni mwa magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, na unasababishwa na bakteria aina ya Leptospira interrogans.

“Ugonjwa huu umekuwepo katika maeneo ya kitropiki ambayo ni yenye hali ya joto katika mabara ya Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kusini, Afrika, Asia na Australia, wanyama aina za panya, kindi, mbweha, kulungu, swala na wanyamapori wengine wameripotiwa kupata maambukizi ya vimelea hivi na kuwa chanzo cha maambukizi kwa binadamu.” amesema Waziri Ummy Mwalimu

Amesema homa ya Mgunda huambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kupitia uchafuzi wa mazingira ikiwemo vyanzo vya maji kutoka katika mkojo wa wanyama wenye maambukizi.

Waziri Ummy amesema mtu anaweza kupata ugonjwa huo kwa Kugusa mkojo au maji maji mengine ya mwili kutoka kwa wanyama wenye maambukizi, Kugusa maji, udongo au chakula kilichochafuliwa na mkojo wa wanyama wenye maambukizi au kunywa maji yaliyochafuliwa na vimelea vya bakteria wa ugonjwa huo huku maambukizi ya ugonjwa huo kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine hutokea kwa nadra.

Amewataka wagonjwa wenye dalili za homa, kuvuja damu, kichwa kuuma na mwili kuchoka kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili wapate matibabu sahihi.