Lugangira awapa ujumbe kikosi kazi cha kuratibu maoni ya demokrasia ya vyama vingi

0
135

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Neema Lugangira ameshauri Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Uchaguzi kupitiwa upya ili kuleta usawa wa kijinsia.

Lugangira amesema hayo wakati akitoa maoni kwa Kikosi Kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan kinachoshughulikia masuala ya demokrasia yaliyoibuliwa kwenye kikao cha wadau kilichofanyika Disemba 15 hadi 17 mwaka jana, jijini Dodoma.

Amesema amelazimika kuwasilisha maoni hayo katika eneo namba nne la kuongeza ushiriki wa wanawake katika siasa kutokana na ukweli kuwa kuna ombwe kubwa.

Mbunge huyo amesema amekiambia kikosi kazi kuhusu changamoto zilizopo kwenye Sheria ya vyama vya Siasa na Sheria ya Uchaguzi ili ziweze kufanyiwa marekebisho na kuendana na wakati wa sasa.

“Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Uchaguzi ni muhimu sana katika kufanikisha lengo la usawa ila kwa sasa haina meno. Mfano Sheria ya Vyama vya Siasa haimpi meno Msajili kufuatilia uwepo wa asilimia fulani ya wanawake ndani ya vyama, hivyo kinachotokea ni utashi wa vyama pekee,” amesema Lugangira.

Ameongeza iwapo Sheria itampa meno Msajili anaweza kuhoji pale ambapo vyama vitashindwa kutekeleza dhana ya usawa wa kijinsia.