Jaji Mkuu asisitiza mahakimu wapya kutochelewesha mashauri

0
133

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amewataka mahakimu wapya kuhakikisha wanatenda haki bila kufungwa na kanuni za kiufundi.

Profesa Juma amesema hayo mara baada ya kuwaapisha mahakimu wakazi wapya 20 katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salam, na kueleza kuwa wananchi wanaokwenda mahakamani wanakwenda kutafuta haki hivyo hawapaswi kuikosa pasi sababu yoyote ya kiufundi.

Aidha, amesisitiza kuwa kila shauri linalokuja mbele yao wanapaswa kulipa uzito bila upendeleo wowote kwa kuzingatia misingi ya haki na uhuru wa mtu.

Pia amesisitiza umuhimu wa maadili kuwa ni kiini cha haki kwani wakitumia uwezo wako wa kujua sheria kupindisha haki watakuwa wameenda kinyume na maadili. “Tutaendelea kufuatilua utendaji kazi wenu na maadili yenu hivyo pale unapokuwa mahakamani mtambue kuwa mna wajibu.”

Pamoja na mambo mengine Jaji Mkuu amewataka mahakimu hao kuhakikisha wanajiendeleza kitaaluma ili wasipoteze uwezo katika utaoji haki na maamuzi ya mashauri mbalimbali.

Kuhusu suala la utoaji wa hukumu amewataka kutojijengea muda wa kutoa hukumu wanavyojisikia wenyewe na kusababisha wananchi kupata adha ya shauri lake kutosikilizwa kwa wakati.