Mo Farah afichua alivyoingizwa Uingereza Kinyemela

0
228

Mwanaridha Sir Mo Farah amefichua kuwa alisafirishwa kwenda Uingereza kinyume na sheria akiwa mtoto na kulazimishwa kuwa mfanyakazi wa ndani.

Nyota huyo wa mashindano ya Olimpiki amesema kuwa watu waliomsafirisha kutoka Djibouti ndio waliompa jina la Mohamed Farah, na kwamba jina lake halisi ni Hussein Abdi Kahin.

Amesema alisafirishwa kutoka taifa hilo la Afrika Mashariki akiwa na umri wa miaka tisa na mwanamke ambaye hakuwa amewahi kumuona kabla, na kufanywa mwangalizi wa watoto wa familia nyingine.

Awali aliwahi kunukuliwa akisema kuwa alikwenda Uingereza akitokea Somalia na wazazi wake kama wakimbizi.

Lakini katika taarifa yake ya hivi karibuni akifanya mahojiano na BBC amesema kuwa wazazi wake hawajawahi kufika Uingereza, na kwamba mama yake na kaka zake wawili wanaishi Somaliland, eneo linalopigania uhuru wake kutoka Somalia.

Ameongeza kuwa, baba yake aliuawa akiwa na miaka minne katika mgogoro huko Somalia, na kwamba alipofikisha umri wa miaka nane au tisa alichukuliwa kwenda Djibouti, na ndipo alipochukuliwa na kupelekwa Uingereza, akilaghaiwa kuwa anakwenda kuishi na ndugu zake.

Katika kipindi chote cha makuzi yake amesimulia kuwa alipitia changamoto nyingi ikiwemo manyanyaso ya kunyimwa chakula na uhuru wa kuzungumza.