Rais Samia Suluhu Hassan amesema jitihada zaidi na ushitikiano madhubuti unahitajika ili kufanikisha suala la utunzaji wa mazingira barani Afrika.
Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo kwenye mkutano wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati (AMECEA) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere mkoani Dar es Salaam.
Amesisitiza kuwa wajibu wa kutunza mazingira ni wa kila binadamu, hivyo ni vema watu wote wakashiriki katika kutunza mazingira.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema hata vitabu vya dini vinasisitiza utunzaji wa mazingira, na hivyo kuwaomba viongozi wa dini kushirikiana na serikali katika kuandaa mikakati ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
“Ndugu viongozi wa dini niwaombe sana kuendelea kushirikiana na serikali kama mnavyofanya sasa katika kuendeleza mapambano ya uharibifu wa mazingira kwa kuwa hata katika biblia kitabu cha Mwanzo sura ya 2:5 Mungu ameamrisha kulinda ardhi bila kuchoka.” amesema Rais Samia
Aidha, amesema magonjwa mengi ya mlipuko hutokea kutokana na uchafu unaosababishwa na kutotunza mazingira, huku akiitaka sekta binafsi kuiga mfano wa viongozi wa dini katika kuwa mstari wa mbele kwenye juhudi za kutunza mazingira.
Rais ametoa wito kwa viongozi mbalimbali katika maeneo yao kuhakikisha wanasimamia suala la utunzaji wa mazingira bila kuchoka.
Pia amelipongeza jiji la Dar es Salaam kwa kushika nafasi ya sita kwa usafi Barani Afrika.