Rais wa Sri Lanka, Gotabaya Rajapaksa amethibitisha kuwa atajiuzulu, ofisi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo imeeleza.
Hatua hiyo inakuja siku mbili baada ya waandamanaji kuvunja na kuingia katika makazi rasmi ya viongozi hao huku wakikataa kuondoka hadi hapo (viongozi) watakapojiuzulu.
Hata hivyo, mapema spika wa bunge alikuwa ameeleza kwamba Rais atajiuzulu Julai 13 mwaka huu.
Taarifa za awali kuhusu kujiuzulu kwa kiongozi huyo ambaye haifahamiki kwa hakika alipo, ilitolewa Jumamosi, hata hivyo wananchi waliipokea kwa mashaka, wakiwa na wasiwasi kwamba huenda asikubalia kuachia madaraka.
Kwa mujibu wa katiba ya Sri Lanka, kujiuzulu kwa Rais kutakuwa halali endapo ataandika barua imfikie spika wa bunge.
Taifa hilo la Kusini mwa Asia linapitia kipindi kigumu cha mdororo wa uchumi ambapo limeshindwa kuingiza nchini humo huduma za msingi kwa ajili ya wananchi kama vile mafuta.