Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imekubali ombi la Halima Mdee na Wenzake 18 la kufungua kesi ya kupinga uamuzi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuwavua uanachama wa chama hicho.
Mahakama imetoa uamuzi wa kukubali ombi hilo mbele ya Jaji Mustapha Ismail baada ya kupitia hoja za mawakili wa wabunge hao ya kuomba ridhaa ya kufungua shauri hilo kupinga kuvuliwa uanachama wa CHADEMA.
Licha ya Mahakama kuridhia maombi ya Mdee na wenzake, mawakili wa CHADEMA wakiongozwa na Peter Kibatala wamepinga hoja za mawakili wa Mdee na wenzake kwa kile walichodai hazijakidhi vigezo vya kisheria kupewa ridhaa ya kufungua shauri hilo.
Hata hivyo Jaji Ismail katika uamuzi wake amekubaliana na vigezo na hoja zote za mawakili wa Mdee na Wenzake 18 zilizowasilishwa na jopo la mawakili wanne likiongozwa na Ipilinga Panya,
Kutokana na uamuzi huo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa siku 14 kwa Mdee na wenzake 18 wawe wamefungua shauri lao mahakamani hapo kwa mujibu wa sheria.