Samaki mkubwa atupwa baada ya kuvuliwa

0
127

Samaki aina ya Popoo -Sunfish mwenye uzito wa kilo 142 na urefu wa sentimita 120 ambaye alivuliwa tarehe tatu mwezi huu katika kina kirefu cha bahari huko mkoani Mtwara, ametupwa dampo.

Afisa uvuvi wa manispaa ya Mtwara – Mikindani Karim Mzee amesema kuwa, wamefikia uamuzi huo baada ya samaki huyo mkubwa wa ajabu ambaye haliwi kuanza kutoa harufu mbaya.

Amesema walifanya mawasiliano na maafisa wa Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Bahari (TAFIRI), lakini hawakupata majibu yaliyoeleweka.

Ameongeza kuwa maafisa wa TAFIRI wameshindwa kwenda mkoani Mtwara kwa ajili ya kumchukua samaki huyo kwa madai ya kukosa usafiri.

Ameongeza kuwa samaki aina hiyo aliwahi kuvuliwa mwaka 2020, lakini hakuwa mkubwa kama wa mwaka huu ambaye naye alitupwa.

Samaki huyo alivuliwa na wavuvi wa hiari ambao hutega nyavu baharini ambazo hubeba chochote kilichopo baharini.

Kwa upande wao baadhi ya wavuvi wamesema wao wamekuwa wakivua muda mrefu na jana ndio wamemuona samaki huyo kwa mara ya kwanza na kwa kimuonekano hana nyama ila ana mafuta mengi sana na kwamba akiachwa kwenye jua muda mrefu anapotea kabisa.

Wamesema kuwa samaki huyo hujulikana kama mola mola au nyuani na haliwi na hachelewi kuoza.