Shaka afanya ziara JKCI

0
104

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shaka Hamdu Shaka amefanya ziara katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo akiwa kwenye ziara hiyo amepata nafasi ya kupokea taarifa zinazohusu taasisi hizo.

Aidha Shaka amepata nafasi ya kuzungumza na Wananchi mbalimbali waliokuwa wakipatiwa huduma mbalimbali.Pia katika ziara hiyo amezungumza na baadhi ya raia wa nchi mbalimbali za Afrika wakiwemo wa Rwanda,Burundi na Congo ambao wamekuja kupata huduma za matibabu ya afya.

Shaka amefanya ziara hiyo leo mchana na lengo la ziara yake pamoja na mambo mengine ilikuwa ni kwenda kumjulia hali mzazi wa Watoto mapacha waliotengenishwa Amina Amosi(18) Mkazi wa Simiyu aliyepo Hospitalini hapo.

Amemtia moyo huku akitoa maelekezo kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii kutembelea mzazi huyo na kumueleza namna ambavyo Serikali itamsaidia malezi ya Watoto.

Akiwa katika ziara hiyo Shaka amepokea taarifa ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya ikiwemo ununuzi wa vifaa tiba pamoja na uwekezaji katika miundombinu.