Msomera wapata Mawasiliano ya simu

0
156

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema zoezi la kuboresha huduma za Mawasiliano katika makazi mapya ya wananchi waliohama kutoka Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera litawafanya waweze kupata taarifa mbalimbali duniani kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Waziri Nape ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa upatikanaji wa huduma za Mawasiliano pamoja na maendeleo ya zoezi la ukusanyaji wa taarifa za Watu na Makazi katika kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga ambako wakazi wapya kutoka Ngorongoro wanaishi.

Sambamba na hayo Waziri Nape ameongeza kuwa Utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ni jambo endelevu na hivyo aliongozana na wataalam wa Wizara yake ili kuhakikisha Msomera inawekewa mfumo huo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma nyingine za kijamii na kuifanya Msomera kuwa Kijiji cha Kidijitali.

Serikali imekuwa ikitoa hamasa kwa jamii ya kabila ya Wamasai kuhama kwa hiari kutoka Ngorongoro na kwenda katika Kijiji cha Msomera kilichopo wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, ili kutunza mazingira kwani jamii hii asili yao ni ufugaji na kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa ikiongezeka kwa kasi na kuongezeka kwao pamoja na mifungo yao na hivyo kunahatarisha mazingira ya hifadhi ya Loliondo.