Ureno kushirikiana na Tanzania kujenga bandari ya uvuvi

0
166

Tanzania na Ureno zimekubaliana kukuza ushirikiano uliopo hasa katika sekta ya uchumi wa buluu kwa kutumia rasilimali za bahari.

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mazungumzo ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango na Rais Marcelo Rebelo de Sousa wa Ureno, mazungumzo yaliofanyika Ikulu ya nchi hiyo mjini Lisbon.

Dkt. Mpango amemueleza Rais huyo wa Ureno kuwa, lengo la serikali ya awamu ya sita ni kukuza uchumi wa buluu kwa kutumia vema bahari na rasilimali zake.

Pia amesema Tanzania imeweka mikakati ya kujenga bandari ya uvuvi katika bahari ya Hindi pamoja na ziwa Victoria na Tanganyika itakayochangia katika kuongeza mapato katika sekta hiyo.

Kwa upande wake Rais Marcelo Rebelo de Sousa amesema Ureno ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kujenga bandari ya uvuvi, itakayosaidia Tanzania kunufaika zaidi kupitia rasilimali za bahari na kuimarisha uchumi wa buluu.

Ameongeza kwamba Ureno ipo tayari kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha inapiga hatua za kimaendeleo katika uchumi wa buluu pamoja na kukuza sekta ya biashara na uwekezaji.

Makamu wa Rais yupo nchini Ureno kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhifadhi wa bahari na rasilimali zake, wenye lengo la kuhamasisha juhudi za mataifa katika kufanikisha utekelezaji wa lengo la 14 la maendeleo endelevu.