Bajeti ijayo kupangwa kutokana na ripoti ya sensa

0
110

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson amesema, bajeti ya mwaka wa fedha wa 2023/2024 itapangwa kutokana na takwimu zitakazopatikana kwenye sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu.

Kutokana na umuhimu wa sensa hiyo, Spika ametoa wito kwa watanzania kushiriki kikamilifu katika sensa, ili kuisaidia serikali kupanga bajeti itakayokuwa na uhalisia wa taarifa ya idadi ya watu

Dkt. Tulia ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa kongamano la viongozi wa dini kuhusu sensa ya watu na makazi, ambapo yeye alikuwa mgeni rasmi.

Ameongeza kuwa sensa ya watu na makazi itasaidia katika kutoa dira ya maendeleo kwa miaka ijayo kwa kuzingatia mahitaji ya watu, hivyo ni.muhimu watanzania wote wakashiriki.

Spika amewashukuru viongozi wa dini kwa kuandaa kongamano hilo na kuwa wasemaji wazuri katika kuhamasisha waumini wao na watanzania kujiandaa kuhesabiwa.

Amewataka viongozi hao waendelee kuhamasisha zoezi la sensa katika nyumba za ibada, ili jamii izidi kufahamu umuhimu wake.

“Niwapongeze sana viongozi wa dini kwa kuona umuhimu wa sensa ya watu na makazi, na hii leo mmethibitisha kuwa suala la sensa lipo kimaandiko kwenye vitabu vya dini na hivyo ni wajibu wenu kuwakumbusha waumini kujiandaa kikamilifu kuhesabiwa.” amesisitiza Dkt. Tulia.