Bodi mpya Ocean Road yafundwa

0
122

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameitaka Bodi mpya ya wadhamini katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kusimamia ubora wa huduma zinazotolewa katika Taasisi hiyo pamoja na kuweka mfumo mzuri wa kushughulikia malalamiko ya wananchi.

Waziri Ummy amesema hayo leo kwenye hafla fupi ya kuzindua Bodi mpya ya Wadhamini ya Taasisi hiyo Jijini Dar Es Salaam.

“Bodi mpya ya Wadhamini nataka mtambue kwamba mnayo kazi kubwa mbele yenu ya kuhakikisha Taasisi inatoa huduma zenye kiwango chenye Ithibati za Kimatafa tukiwa na lengo la kuhakikisha wananchi wetu wanapata huduma bora za kibingwa na kibobezi za Saratani hapa nchini” amesema

Waziri Ummy pia ameitaja miradi ambayo Bodi hiyo inatakiwa kuisimamia ili iweze kukamilika na kutoa huduma bora ikiwemo, Miradi ya ujenzi pamoja na usimikaji wa mashine mpya ya kisasa ya uchunguzi wa saratani (PET CT Scan) pamoja na kiwanda cha Cycloton vyote kwa pamoja vikigharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 18.2 ambapo ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi huu Juni 2022 na usimikaji wa mashine kuanza mwezi ujao.

Ametaja miradi mingine kuwa ni ukarabati na usimikaji wa mashine mpya za MRI, Digital X-Ray, ukarabati wa jengo na ununuzi wa vifaa vya wodi ya wagonjwa mahututi (ICU), kukarabati na kusimika vifaa kwa ajili ya huduma za tiba mtandao (Telemedicine) zitakazogharibu Shilingi Bilioni 5.4 kutoka kwenye fedha za UVIKO-19.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi iliyomaliza muda wake Prof. Hamis Dihenga amesema katika kipindi cha uongozi wa Bodi yake waliweza kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi wa Serikali hivyo kuiwezesha Bodi kufanya kazi ambayo imeweza kuleta tija katika kuboresha huduma za tiba ya Saratani nchini.

“Katika kipindi cha uongozi wa bodi yangu tuliweza kuongeza huduma za tiba ya saratani kutoka aina mbili hadi kufikia kutoa tiba za aina sita za saratani” amesema Prof. Dihenga.

Naye, Prof. Ephata Kaaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Wadhamini wa taasisi hiyo ameahidi kuendeleza mazuri yote yaliyofanywa na Bodi iliyomaliza muda wake.