Mkutano wa Jumuiya ya Madola waanza Kigali

0
152

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango leo ameshiriki kwenye ufunguzi wa mkutano wa 26 wa wakuu wa serikali wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGMU 2022) unaoendelea Kigali, Rwanda.

Makamu wa Rais anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo unaofanyika kwa muda wa siku mbili.

Mkutano huo umetanguliwa na mikutano mbalimbali iliyojikita katika vipaumbele vya kisera ikiwa ni pamoja na utawala bora, utawala wa sheria na haki za binadamu, vijana, afya, teknolojia na uvumbuzi pamoja na maendeleo endelevu katika biashara na uchumi.

Akihutubia mkutano huo Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema Jumuiya ya Madola inapaswa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza duniani na sio kuchagua maeneo ya kutatua changamoto hizo.

Ameongeza kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola hazina budi kutambulika kwa utawala bora na utawala wa sheria pamoja na ulinzi wa haki.

Kwa upande wake katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Patricia Scotland amesema, mkutano huo ni fursa kwa mataifa kuunganisha mawazo na kutoa ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili dunia hasa za kiuchumi zilizosababishwa na janga la UVIKO -19, mabadiliko ya tabianchi pamoja na migogoro iliyosababisha kupanda kwa gharama za chakula na nishati ya mafuta duniani.

Amesema nchi wanachama zinapaswa kuaminiana na kusikilizana kwa manufaa ya wananchi bilioni 2.5 waliopo katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.