Wakazi wapya wa kijiji cha Msomera kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga waliohamia kutoka Ngorongoro, wameipongeza serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya huduma za jamii katika eneo hilo.
Pongezi hizo zimetolewa na baadhi ya wakazi hao mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea kijijini hapo kwa lengo la kukagua makazi na miundombinu ya huduma za jamii inayojengwa katika eneo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake mkazi mpya wa kijiji hicho Richard Tobiko Ole Mokoro amesema kuwa yaliyofanyika katika kijiji hicho ni upendeleo ambao hawakuutegemea.
“Kule Ngorongoro tulikuwa tunanywesha ng’ombe inapita siku moja hatunyweshi, lakini huku tumekuta maji ni mengi kila siku wanakunywa maji.” na kuongeza kuwa
“Tunamshukuru sana Rais Samia, sasa tumepata uhuru, tumepata hatma ya maisha yetu, kwa sasa mtu unaweza kufanya chochote ambacho unataka kufanya, tofauti na ilivyokuwa Ngorongoro.” amesema Richard Tobiko Ole Mokoro
Kwa upande wake Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa, idadi ya wananchi wanaojiandikisha kuhamia Msomera imeendelea kuongezeka siku hadi siku.
“Serikali yenu ni aminifu, wakati tunaanza kutekeleza hili watu hawakuwa wanaamini na ninyi mnajua upendo aliokuwa nao Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za kuja kuwahudumia.”
“Mlipokuja hapa mmeona wenyewe, mmepata nyumba pamoja na hati, shule ya msingi na sekondari ipo hapa, miradi ya maji inajengwa, tunajenga barabara, tunajenga kituo cha afya, huduma hizi ni za wote.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa
Aidha, Waziri Mkuu amewapongeza wajenzi wa nyumba katika kijiji cha Msomera kwa kutekeleza zoezi hilo kwa viwango na kasi kubwa.
“Tuliweka malengo ya kujenga nyumba 103 na zote tayari zimekamilika na ujenzi wa nyumba nyingine zilizobaki ili kufikia idadi ya nyumba 500 unaendelea.” amesema Waziri Mkuu
Awamu ya pili ya zoezi la kuhamisha wakazi wa eneo la Ngorongoro kwa hiari lilianza tarehe 20 mwezi huu ambapo jumla ya kaya 27 zenye watu 127 na mifugo 488 watahamishwa, kaya 1 kati hizo itahamia Karatu.