Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema Serikali itaendelea kuyalinda, kuyasimamia, kuyatangaza na kuyaboresha maeneo ya Makumbusho ya Wapigania Uhuru ili kuyafanya yawe vivutio vya utalii.
Ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu maswali kuhusu namna ya kukarabati miundombinu na kuboresha makumbusho ya wapigania uhuru.
Amesema kupitia fedha za UVIKO-19 kiasi cha shilingi bilioni 2.45, Serikali itakarabati miundombinu ya barabara na kuboresha maeneo ya Makumbusho na Malikale ili kuvutia watalii.
Akifafanua kuhusu ujenzi wa barabara ya kwenda Kituo cha Makumbusho ya Mkwawa, amesema, Wizara ya Maliasili na Utalii itashirikiana na wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) wa mkoa wa Iringa kuifanyia ukarabati barabara hiyo.
Aidha, kuhusu ukarabati wa Jengo la Chifu Adam Sap Mkwawa amesema Wizara inaendelea kufanya mazungumzo na familia husika ili litumike kwa ajili ya kuhamasisha Utalii.