Mhandisi Kundo : Watu wenye ulemavu lazima wahabarishwe

0
162

Serikali imevitaka vyombo vya habari vya televisheni ambavyo bado havina wakalimani wa lugha za alama katika vipindi na ziara za viongozi wa kitaifa kuhakikisha wanatimiza sheria ya kuwepo wakalimani wa lugha hizo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge Khadija Taya aliyetaka kufahamu ni lini uwepo wa wakalimani wa lugha za alama kwa vipindi vya habari vya televisheni na ziara za viongozi utakuwa wa lazima.

Naibu Waziri Kundo amesema mwaka 2018 sheria na kanuni ziliwekwa kwamba vyombo vya habari vinatakiwa kuwa na wakalimani wa lugha za alama na kwamba baadhi ya televisheni tayari zimetii sheria hiyo na ambavyo bado vinatakiwa kufanya hivyo.

Aidha Mhandisi Kundo ameitaka mamlaka inayosimamia vyombo vya habari kuhakikisha wanawakumbusha wamiliki wa vyombo hivyo na wanaoratibu makongamano na matukio ya viongozi kuhakikisha wanatimiza wajibu huo kwa kuwa ni takwa la kisheria.