Wahamiaji kusakwa Loliondo

0
210

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini Dkt. Anna Makakala ametangaza kuanza kwa operesheni maalum ya siku kumi kusaka wahamiaji katika eneo la Loliondo, Ngorongoro mkoani Arusha.

Dkt. Makakala ametangaza kuanza kwa operesheni hiyo akiwa Loliondo na kuongeza kuwa operesheni hiyo itafanyika pamoja na zoezi linaloendelea la uwekaji wa alama za mipaka katika pori tengefu la Loliondo.

Amesisitiza kufuatwa kwa sheria pale wageni wanapotaka kuingia au kutoka nchini, na kwamba Uhamiaji imejipanga vema kusimamia eneo hilo katika mipaka yote nchini.

“Nchi yetu imebarikiwa kwa kuwa na maeneo mazuri ambayo yanavutia wahamiaji kufika nchini kwa sababu tofauti, hatutakubali hilo litokee wakati wowote ule,” amesema Dkt. Makakala

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala amemfahamisha Dkt.Makakala kuwa wilaya yake inaendelea vema na utekelezaji wa zoezi la uwekaji wa alama za mipaka katika eneo la pori tengefu la Loliondo na kwamba atatoa ushirikiano katika zoezi la kusaka wahamiaji ili wale wote watakaobainika wachukuliwe hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi.