Wakandarasi wazawa wapewa somo

0
187

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewaasa wakandarasi wazawa kutumia vema na kwa ufanisi fursa wanazopewa na serikali za ujenzi wa miradi mbalimbali, ili kuendelea kupewa nafasi hizo.

Makamu wa Rais amesema hayo aliposimama na kukagua ujenzi wa daraja la Nyeburu linalounganisha eneo la Pugu na Chanika mkoani Dar es Salaam, ambalo ujenzi wake umekuwa ukisuasua.

Ameonesha kutofurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo kwa kuwa umechukua muda mrefu, na hivyo kuleta adha kwa wananchi hasa wakati wa mvua.

Dkt. Mpango amesema serikali imeendelea kuwapa kipaumbele wakandarasi wa ndani kutokana na kutambua wanafahamu vema changamoto zinazosababishwa na ubovu wa miundombinu, na kwamba wanapaswa kutekeleza majukumu yao kiufanisi.

Pia ameuagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) pamoja Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuwasimamia kikamilifu wakandarasi ili wakamilishe miradi kwa wakati.