Kiongozi Mkuu wa madhehebu ya Kiislamu ya Mabohora duniani Sheikh Syedna Mufaddal Saifuddin amewasili nchini ambapo kwa muda wa wiki mbili atakazokuwa hapa nchini pamoja na shughuli za kiimani anatarajiwa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.
“Hapa nchini amekuja kuunga mkono malengo ya Royal Tour na yeye mwenyewe na wafuasi wake watakwenda mapumziko katika maeneo mbalimbali. Pia, iwapo taratibu zitakamilika na akaridhia anaweza kufanya mhadhara wake mkubwa wa kidini hapa nchini Julai ambapo wafuasi wake kati ya 30,000 hadi 40,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani humfuata na tunajipanga ikitokea hivyo tutawaonesha watu hao na mabohora wengine duniani filamu ya Royal Tour,” amesema Zainuldeen Adamjee – mmoja wa viongozi wa dhehebu hilo nchini
Akimpokea Kiongozi huyo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amesema amewasilisha kwa kiongozi huyo Mkuu wa madhehebu ya Kiislamu ya Mabohora duniani Sheikh Syedna Mufaddal salamu za Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo utayari wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mhadhara mkubwa wa mwaka wa kiongozi huyo utakaoleta maelfu ya watu hapa nchini.