Siku ya Mtoto wa Afrika yaadhimishwa leo

0
105

Watoto wa Tanzania leo wanaungana na wenzao wa mataifa mbalimbali ya Afrika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika.

Chimbuko la maadhimisho hayo ni azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) kwa sasa AU mwaka 1990 kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini waliouawa Juni 16 mwaka 1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.

Watoto hao walikuwa wakidai haki zao za kutobaguliwa pamoja na haki nyingine za kibinadamu ikiwemo ya kupata elimu bora na hivyo kupinga mifumo ya elimu ya kibaguzi.

Kufuatia tukio hilo, OAU iliazimia kuwa tarehe 16 Juni ya kila mwaka iwe siku ya Mtoto wa Afrika ambapo kupitia maadhimisho hayo Serikali za nchi za Afrika na wadau wengine wanakumbushwa kuandaa mipango thabiti ya kuwaendeleza watoto na kukuza ufahamu wa wazazi, walezi na jamii kuhusu utatuzi wa changamoto zinazowakabili watoto wa Afrika na kuzitafutia ufumbuzi. 

Maadhimisho hayo pia ni fursa ya kutathmini utekelezaji wa sera zinazohusu maendeleo ya watoto kwa kuwapatia huduma stahiki ikiwa ni pamoja na afya, elimu, ulinzi na malezi bora ili kuwarithisha stadi mbalimbali na tunu za kitaifa kwa manufaa yao, familia na taifa kwa ujumla.

Kauli mbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka huu ni Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa Watoto.

Kauli mbiu hiyo inawataka wazazi, walezi, Serikali na wadau wengine kuzingatia wajibu wao katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na maendeleo ya mtoto ili aweze kudhibiti changamoto ya ongezeko la vitendo vya ukatili pamoja na kutoa haki sawa kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.