Msanii wa Nigeria kurekodi filamu kwenye vivutio vya Tanzania

0
128

Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Francis Michael amekutana na kufanya mazungumzo na Msanii Nguli wa Filamu kutoka nchini Nigeria, James Ikechukwu maarufu Jim lyke, na kukubaliana kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko nchini Tanzania kupitia filamu.

Kikao hicho kimefanyika leo katika Ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dodoma.

“Ninakupa fursa ya kutumia hifadhi zetu unapotengeneza filamu yako ili kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania,” Dkt. Michael amesisitiza.

Aidha, amemtaka msanii huyo kutembelea vivutio vya utalii vilivyoko nchini akitolea mfano wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ni hifadhi bora Afrika, ili ajionee Tanzania ilivyobarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii.

Kwa upande wake Jim lyke amemshukuru Dkt. Michael kwa kumpatia fursa hiyo na kusema kuwa anatarajia kutengeneza filamu itakayoshirikisha wasanii wa hapa nchini na kwamba atahakikisha anatumia zaidi vivutio vinavyoongoza na kutambulika zaidi duniani.