Wanaohama Ngorongoro kwa hiari wamshukuru Rais

0
177

Wakazi wa tarafa ya Ngorongoro mkoani Arusha ambao wameamua kuhama kwa hiari kwenye eneo la hifadhi ya Ngorongoro wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa upendo aliouonesha kwao kwa kuhakikisha nao wanakuwa na makazi ya kudumu eneo la Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga.

Wakizungumza huku wakiwa wanaezua nyumba zao tayari kwa kuhama katika eneo hilo kwa hiari, wakazi hao wamesema walikuwa wanaisubiri fursa hiyo kwa muda mrefu lakini Rais Samia ameitekeleza, hivyo wanamshukuru kwa uamuzi wake.

Mkazi wa kijiji cha Kimba wilayani Ngorongoro, Beatrice Soka amesema amefurahi kuhama kwa sababu kwa muda mrefu walitamani mchakato huo ufanyike lakini ulichelewa.

“Kwa hiyo tamko hili lilipoletwa kwa kweli mimi ni miongoni mwa watu tuliojiandikisha kwa hiari pamoja na familia yangu kwa ajili ya kwenda huko Msomera.” amesema Beatrice na kuongeza kuwa

“Bahati nzuri nimekwenda huko Msomera na nimerudi jana. Nimeshuhudia kwa macho yangu na akili zangu kwa kweli fursa tuliyopewa na Rais Samia ni ya kipekee, ni ajabu, ni fursa ya upendeleo kwa wana Ngorongoro wote”.

“Kuna shule, huduma ya maji , miundombinu yote na kuna mabwawa ya kutosha, nyumba, mzunguko wa nyumba kuna ekari tatu mbali na mashamba yalipo nje ya pale ekari tano, na mama Samia ametuwezesha tuliotoka hapa tuweze kwenda kuendelea na kasi kwani tumepoteza muda”. amesema mkazi huyo wa Ngorongoro , Beattice Soka

Kwa upande wake Pasihaya Parakoi Seseka ambaye ni miongoni mwa wakazi wa tarafa ya Ngorongoro ambaye amuamua kuhama kwa hiari amesema, hiyo ni fursa kwao ya kupata maendeleo, kwani maeneo wanayopelekwa ni mazuri kwa shughuli za maendeleo.

Akizungumza baada ya kushuhudia zoezi hilo mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongella amesema zoezi hilo ni la hiari na walioamua kuondoka wamefikia hatua hiyo baada ya kujadiliana na familia zao na kuafiki mpango huo bila kulazimishwa.