Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba leo amewasilisha bungeni jijini Dodoma bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 ambapo shilingi trilioni 41.48 zitatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida pamoja na maendeleo.
Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma Dkt. Nchemba amesema kuwa kati ya fedha hizo shilingi trilioni 26.48 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwa ni asilimia 63.8 ya bajeti yote ikijumuisha shilingi trilioni 11.31 kwa ajili ya ulipaji wa deni la serikali na gharama nyingine za Mfuko Mkuu.
Ameongeza kuwa shilingi trilioni 9.83 ni kwa ajili ya mishahara ikiwemo nyongeza ya mshahara, upandishaji wa madaraja kwa watumishi na ajira mpya.
Dkt. Nchemba amesema dhima kuu ya bajeti ya mwaka 2022/2023 kama ilivyokubaliwa na nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kuongeza kasi ya kufufua uchumi na kumarisha sekta za uzalishaji.
Amesema Katika utekelezaji wa dhima
hiyo kwa mwaka 2022/2023 kipaumbele kitakuwa katika sekta za uzalishaji zikiwemo Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Nishati, Uwekezaji na Biashara.
Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, lengo la serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti
wa CCM ni kujenga uchumi, kukabiliana na
umaskini pamoja na ukosefu wa ajira hasa kwa vijana.