CHADEMA yaweka pingamizi dhidi Mdee na wenzake

0
287

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewawekea pingamizi mahakamani wabunge 19 wa viti maalum, waliovuliwa uanachama wa chama hicho ambao kwa pamoja wamefungua maombi kupinga kufukuzwa uanachama wao, huku kikiwasilisha hoja sita.

Pingamizi hilo limewsilishwa leo katika Mahakama Kuu ya Tanzania na mawakili wa CHADEMA wakiongozwa na Peter Kibatala mbele ya Jaji John Mgetta wa mahakama hiyo.

Wabunge hao wakiongozwa na Halima Mdee walifungua maombi Mahakama Kuu dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA, wakiomba kibali cha kufungua shauri la mapitio ya kuhusu uamuzi huo wa kuvuliwa uanachama.

Katika hoja zao, mawakili wa CHADEMA imesema mahakama haina mamlaka kusikiliza maombi ya wabunge hao kwa kwa sababu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haiwezi kuchunguzwa kwa jambo lolote ililolifanya.

Pia wamebainisha kuwa mahakama haina mamlaka kusikiliza maombi ya mapitio ya kimahakama dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema kwa sababu si chombo cha umma.

Hata hivyo mawakili wa wabunge hao wamepinga hoja zilizowasilishwa na CHADEMA kupitia mawakili wake wakidai hoja hizo hazina mashiko.

Baada ya kusikiliza hoja za mawikili wa pande zote mbili Jaji Mgeta ameahirisha shauri hilo hadi Juni 22 mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi huku akiwaamuru wabunge hao kuendelea na nyadhifa zao hadi uamuzi utakapotolewa na mahakama katika tarehe iliyopangwa.