Aliyeng’olewa Umeya Moshi achukua tena fomu

0
122

Juma Raibu Meya wa zamani wa manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro aliyevuliwa wadhifa huo baada ya kupigiwa kura na madiwani za kukataliwa, amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania tena nafasi hiyo.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu katika ofisi za CCM Moshi Mjini, Raibu amesema ameamua kurudi kuwania nafasi hiyo baada ya kuona kuwa toka ameondolewa kwenye nafasi hiyo Moshi imepoa na haijachangamka kama nyakati alivyokuwa yeye.

Amesema zaidi ya wananchi 500 walifika nyumbani kwake kumuomba na kumchangia ili aweze kurudi kugombea nafasi hiyo.

Juma Raibu aling’olewa katika wadhifa wa Meya wa manispaa ya Moshi Aprili 11 mwaka huu baada ya madiwani kupiga kura za siri na kati ya kura 28 zilizopigwa, 18 zikitaka asiendelee na wadhifa huo na 10 zikimtaka abaki katika nafasi hiyo aliyoitumikia tangu mwaka 2020 baada ya uchaguzi mkuu.

Tuhuma zilizomng’oa Raibu madarakani ni pamoja na matumizi mabaya ya ofisi, kujihusisha na vitendo vya rushwa, kuruhusu ujenzi holela na kutumia fedha nje ya utaratibu.