Mradi wa kuchakata gesi kubadili taswira ya uchumi wa nchi

0
216

Rais Samia Suluhu Hassan amesema mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia ujulikanao kama LNG unaotarajiwa kutekelezwa mkoani Lindi ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati ambao ukikamilika utabadili taswira ya nchi kiuchumi.

Rais Samia ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa hafla ya utiliaji saini makubaliano ya awali ya mkataba wa nchi hodhi (HGA) wa mradi wa kuchakata na kusindika gesi.

Ameeleza kwamba mradi huo ni mkubwa hivyo unahitaji nguvu ya pamoja katika kuulinda kwa nguvu zote ili vizazi vijavyo viweze kunufaika na rasilimali ya nchi yao huku akiagiza wizara yenye mamlaka kuhakikisha inaongeza kasi katika tafiti za utafutaji wa gesi maeneo mengine ya nchi.

Aidha, amewataka Watanzania na makampuni binafsi ya wazawa kujipanga kikamilifu kutoa huduma kwenye mradi huo.

Pamoja na mambo mengine Rais amewaagiza wakuu wa mikoa kuwaandaa vijana wa Kitanzania waweze kunufaika kikamilifu na mradi huo.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati, January Makamba amesema makubaliano ya mkataba huo yalianza mwaka 2021 na kwamba utakapokamilika utasaidia kupunguza changomoto ya ajira kwa Watanzania.

Waziri Makamba amesema wzara yake imejipanga kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa kasi kubwa kwa ajili ya kuchochea uchumi shindani ndani ya taifa.

Utekelezaji wa mradi huo unaelezwa kwamba utagharimu shilingi trilioni 70.