Tanzania na Marekani kukuza uhusiano wa kibishara

0
2390

Tanzania na Marekani zimetiliana saini makubaliano ya Itifaki ya maboresho ya usafiri wa anga kwa lengo la  kufungua soko  la  safari za ndege za abiria na mizigo,  ili kupanua fursa za kiuchumi na ajira.
 
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amewaambia waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam kuwa, kusainiwa kwa makubaliano hayo ni muendelezo wa uhusiano wa kibiashara baina ya Tanzania na Marekani.
 
Amesema hatua hiyo inalenga kurahisisha usafiri kwa watalii pamoja na wawekezaji kutoka nchini Marekani  wanaotaka kuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii na kuangalia fursa za uwekezaji na masoko.
 
Naye Balozi wa Marekani nchini Donald Wright amesema, kupitia makubalaino hayo wanatarajia kuongeza kiwango cha watu kusafiri na kufanya biashara, kupanua fursa za ajira na kubadilishana ujuzi ili kukuza uchumi wa mataifa hayo mawili.
 
Itifaki ya Maboresho ya Usafiri wa Anga ni sehemu ya makubalaino ya anga huru yaliyoasisiwa miaka 22 iliyopita,  na kwa kusainiwa kwa Itifaki hiyo ni mwanzo wa utekelezaji wa makubaliano hayo.