Viuatilifu visivyo na ubora vyawaburuza mahakamani

0
110

Watu saba wakazi wa wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kukutwa na mifuko 507 ya viuatilifu visivyo na ubora

Kaimu Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo amesema viuatilifu hivyo vyenye usajili namba  FU/0344 vinadaiwa kuingizwa nchini kutoka Misri na kila mfuko una uzito wa kilo 25.

Mei 18 mwaka huu polisi mkoani Mtwara walifanya operesheni maalum wilayani Tandahimba na kuwakamata watuhumiwa hao Saba kwa makosa ya kupatikana na kusambaza viuatilifu visivyo na ubora.

Baada ya kubaini kuwa kiasi kikubwa cha viuatilifu hivyo tayari kimesambazwa kwa wakulima, jeshi la polisi mkoa wa Mtwara limetoa wito kwa watu wote walio na viuatilifu hivyo aina ya Makonde kutotuvitumia na badala yake wavisalimishe polisi.

Tarehe 7 mwezi huu mkuu wa mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti aliagiza Haroun Rashid Maarifa ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Prosperity 8 Agro Industries Co. Limited iliyoingiza nchini viuatilifu hivyo ajisalimishe polisi ndani ya saa 48.