Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na na Uratibu George Simbachawene amesema serikali imeendelea kupambana na tatizo la uzalishaji, matumizi na biashara ya dawa za kulevya nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Waziri Simbachawene amesema kama ilivyokuwa mwaka uliopita uzalishaji, matumizi na biashara ya dawa za kulevya imeendelea kuwa tatizo duniani na kuleta athari mbalimbali zikiwemo zile za kiuchumi na kijamii
“Bangi na mirungi imeendelea kuwa tatizo nchini, katika mwaka 2021, jumla ya tani 22.74 za bangi zilikamatwa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 72 ya kiasi kilichokamatwa mwaka 2020. Ukamataji huu ulihusisha jumla ya watuhumiwa 9,484. Mirungi iliyokamatwa katika kipindi hicho ilifikia tani 10.93 zikihusisha watuhumiwa 1,395.” amesema Waziri Simbachawene
Kwa upande wa dawa za kulevya zinazozalishwa viwandani, Waziri Simbachawene amesema kwa mwaka 2021 jumla ya tani 1.13 za heroin zilikamatwa.
“Hiki ni kiasi kikubwa kuwahi kukamatwa kwa mwaka mmoja katika historia ya nchi yetu, kiasi hicho ni mara tatu ya kiasi kilichokamatwa mwaka 2020. Aidha, katika kipindi hicho gramu 811.30 za cocaine zilikamatwa.” amesema Waziri Simbachawene
Amesema serikali imeendelea kupanua wigo wa matibabu kwa waraibu wa dawa za kulevya ambapo hadi kufikia mwezi Desemba mwaka 2021 huduma za tiba ya uraibu zilikuwa zikipatikana kwenye vituo 15 vya kutolea tiba kwa waraibu wa heroine na vituo hivyo kwa pamoja vilikuwa vimesajiri waraibu 11,650.
Vituo hivyo vinapatikana katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Mbeya, Songwe, Dodoma, Mwanza na Arusha.