Mahakama yawaachia huru kina Sabaya

0
143

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imewaachia huru aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita baada ya ushahidi uliotolewa na Jamhuri kugubikwa na utata, hivyo kushindwa kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yanawakabili na kuwatia hatiani.

Mbali na sababu hizo, mahakama imegundua kuwa hati ya mashtaka ilikuwa na mapungufu na kuwa ushahidi uliotolewa dhidi yao mahakamani hapo haujaweza kuthibitisha mashtaka hayo.

Wengine walioshtakiwa na Sabaya ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Hata hivyo Sabaya, Nyegu, Aweyo na Msuya wataendelea kubaki mahabusu kwa kuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.

Hiyo ni kesi ya pili Sabaya kushinda ambapo Mei 6 mwaka huu akiwa na wenzake wawili walishinda rufaa iliyokuwa ikisikilizwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, waliyokata kupinga hukumu ya miaka 30 iliyokuwa imetolewa na na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.