Watu 19 wafariki kutokana na ajali Iringa

0
166

Watu 19 wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea kwenye eneo la Changarawe Mafinga mkoani Iringa.
 
Mkuu wa wilaya ya Mufindi,  Saad Mtambule ameiambia TBC kwa njia ya simu kuwa ajali hiyo imetokea saa tisa, usiku wa kuamkia hii leo.
 
Ameelezea mazingira ya ajali hiyo na kusema kuwa majira ya saa 9 usiku lori la mzigo lililokuwa likitoka mkoani Mbeya kwenda Dar es Salaam lilipata ajali katika eneo hilo na polisi wa usalama barabarani walipofika waliwachukua dereva na utingo wake ambao walipata majeraha na kuwapeleka hospitali.


 
Mtambule amesema katika eneo hilo ziliwekwa alama za tahadhari kuonyesha kuna ajali, lakini dereva wa basi dogo aina ya coaster lililokuwa likisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda mkoani Mbeya alipofika katika eneo hilo hakuona alama za hatari zilizowekwa na badala yake akaligonga lori hilo lilikokuwa limeegeshwa barabarani.
 
Kwa mujibu wa Mtambule, baada ya basi hilo dogo kuligonga lori, watu 16 walifariki dunia papo hapo.
 
Ameongeza kuwa wakati askari wa usalama barabarani na wasamaria wema wakiendelea kuokoa majeruhi wa ajali hiyo ya basi dogo, askari wa usalama barabarani walienda eneo la jirani ili kusimamisha magari yaliyokuwa yakipita kwa lengo la kuwafahamisha madereva wa magari yanayopita kuwa eneo hilo kwa muda huo lina hatari na wanatakiwa kupita kwa tahadhari.
 
Mkuu huyo wa wilaya ya Mufindi amesema baada ya askari hao kujitahidi kumsimamisha dereva wa lori lililokuwa likipita kwa muda huo alikaidi amri ya askari na kwenda kwa mwendokasi na kuwaparamia watu waliokuwa wakiendelea na uokoaji,  na hivyo kusababisha vifo vya watu wengine watatu.
 

Amesema majeruhi wawili kati ya saba wa ajali hiyo hali zao ni mbaya na kwamba polisi inamshikilia dereva wa lori aliyekaidi amri ya askari na kwenda kuwagonga watu waliokuwa wakitoa msaada wa uokoaji.
 
Mtambule ametoa wito kwa madereva kuwa waangalifu wawapo barabarani, kuzingatia alama zinazowekwa barabara pamoja na kutia amri za askari pale wanapotakiwa kufanya hivyo.