Rais Samia Suluhu Hassan amepiga marufuku Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwadai kodi za miaka ya nyuma wafanyabiashara na kuwataka kuwa makini na namna wanavyosimamia ukusanyaji wa kodi.
Akizungumza na wananchi wa mkoa wa Kagera katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kaitaba, Rais Samia amesema wafanyabiashara wasisumbuliwe kwa madeni ya miaka ya nyuma bali waachwe wafanye biashara.
“Naweza kuwaelewa kama mtadai kodi ya mwaka mmoja nyuma lakini sio miaka ya nyuma ambayo inawezekana uzembe ulikuwa kwenu nyie ambao mlishindwa kuweka vizuri mahesabu yenu.” amesema Rais Samia
Hata hivyo amewataka wafanyabiashara kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na kuitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania kusimamia vema ukusanyaji wa mapato.
Awali akimkaribisha Rais kuzungumza katika mkutano huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa amewataka wakuu wa mikoa kusimamia uzalishaji wa zao la alizeti ili kukabiliana na uhaba wa mafuta ya kupikia nchini.
Bashungwa amesema hilo ni agizo na hivyo mkuu wa mkoa atakayeshindwa kusimamia zoezi hilo jina lake litapelekwa kwa Rais kwa hatua zaidi.