Serikali yatoa msimamo msamaha kwa wasiojiweza

0
92

Licha ya matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza kuwa na gharama kubwa na yanahitaji tiba wakati wote, serikali imekuwa ikitoa msamaha wa matibabu kwa wagonjwa wanaougua magonjwa hayo ambao wamethibitika kuwa hawana uwezo wa kugharamia matibabu kwa mujibu wa sera ya afya.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na mbunge wa jimbo la Chaani, Juma Usonge Hamad aliyehoji serikali ina mpango gani wa kutoa matibabu bure kwa maradhi yasiyoambukiza kama Kisukari na shinikizo la damu.

Hata hivyo Dkt. Mollel amesema serikali ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa muswada wa bima ya afya kwa wote ambao utawezesha wananchi wote kupata huduma za afya katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini.

Akijibu Swali la nyongeza lililoulizwa na mbunge Usonge aliyehoji usumbufu wanaopata wazee pindi wanapokwenda hospitalini kupata huduma za matibabu, Dkt. Mollel ameendelea kuwasisitiza wataalamu kufuata maagizo yanayotolewa na viongozi ikiwemo kuhakikisha Wazee wanapata matibabu bure katika vituo vya kutolea huduma za afya.