Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa amemhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za Afya katika hospitali za Wilaya , vituo vya Afya na Zahanati zote nchini utakamilika kwa wakati na kwa ubora zaidi ili wananchi waendelee kupata huduma ya afya kwa wakati na kwa ubora zaidi.
Waziri Bashungwa amebainisha hayo Leo Juni 8, 2022, wakati wa mapokezi ya Rais Samia Suluhu Hassan katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamuro, Mkoani Kagera.
“ Mhe. Rais ulituagiza Ofisi ya Rais -TAMISEMI kuwa hutaki kuona majengo ya hospitali yanabaki kuwa maboma, lakini pia ulituelekeza ujenzi wa Hospitali hizi, Vituo vya Afya na Zahanati lazima ukamilike ili wananchi wapate huduma, nikuhakikishie Rais, ujenzi wa miundombinu hii utakamilika kwa wakati na ubora zaidi” amesema Bashungwa
Aidha, Bashungwa amemshukuru Rais Samia kwa kuwekeza fedha kwa ajili ya uboreshwaji wa miundombinu ya kutolea huduma za afya msingi, barabara pamoja na miundombinu ya elimu Msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamiro, Bashungwa amesema miundombinu hiyo inakwenda kuboresha maisha ya wananchi wa Biharamuro na Mkoa wa Kagera kwa ujumla