Bwawa laleta maafa Brazil

0
1055

Vikosi vya uokoaji nchini Brazil vinaendelea kuwatafuta watu walionusurika kufuatia kuvunjika kwa kingo za bwawa moja la maji lililopo kwenye mgodi mkubwa wa chuma wa Vale.

Takribani watu 200 hawajulikani walipo kufuatia tukio hilo lililotokea kwenye jimbo la Minas Gerais.

Habari kutoka nchini Brazil zinasema kuwa maji yaliyochanganyika na tope yamewafunika ardhini mamia ya wafanyakazi wa mgodi huo wa chuma.

Gavana wa jimbo la Minas Gerais, – Romeu Zema amesema kuwa, kuna wasiwasi huenda wafanyakazi wengi wa mgodi huo wa chuma wa Vale wamekufa katika tukio hilo na kwamba mpaka sasa ni watu Tisa tu ndio waliothibitika kufa.

Barabara nyingi za kuingia na kutoka katika mgodi huo mkubwa wa chuma zimeharibiwa na maji yaliyotoka kwa kasi kwenye bwawa hilo, na kufanya kazi ya uokoaji kuwa ngumu.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter,
Rais Jair Bolsonaro wa Brazil amelitaja tukio hilo kama janga la kitaifa na kuongeza kuwa serikali yake inafanya kila linalowezekana ili kuwaokoa watu walionusurika.