Rais wa Senegal na mkuu wa Umoja wa Afrika, Macky Sall, amemwambia rais wa Urusi Vladimir Putin kwamba azingatie athari za uhaba wa chakula kwa bara la Afrika zinazosababishwa na mzozo wa Ukraine.
Marais hao wawili wamekutana katika mji wa kusini mwa Urusi wa Sochi.
Rais Sall amesema kwamba Rais Vladimir Putin atalazimika “kufahamu kwamba nchi zetu, hata kama ziko mbali na mzozo huo, pia ni waathirika katika ngazi ya uchumi” kutokana na mzozo huo.
Ameongeza kuwa umuhimu wa chakula unapaswa kuwa nje ya vikwazo vya Magharibi kwa Urusi. Kabla ya mzozo huo, zaidi ya 40% ya ngano inayotumiwa barani Afrika ilitoka Ukraine au Urusi.
Kabla ya kuondoka Senegal, ofisi ya rais Sall ilisema ziara hiyo ililenga kukomboa akiba ya nafaka na mbolea ambayo kwa sasa imezuiwa katika bandari za Ukraine.
Nchi za Afrika zinaathirika haswa kutokana na kupanda kwa bei kunakosababishwa na vita. Hapo awali, shirika la habari la Reuters lilinukuu Kremlin ikisema kwamba Putin atatoa maelezo ya kina kuhusu kile kinachotokea kwa nafaka ya Ukraine.
Katika hotuba yake kwa umma baada ya mkutano huo, iliyonukuliwa na AFP, Putin alisema Urusi siku zote iko upande wa Afrika.