Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Profesa Elisante Ole Gabriel amesema, tuzo za tathmini ya utendaji kazi iliyotolewa kwa wakuu wa idara ya usimamizi na utawala wa rasilimali watu itasaidia kuongeza nguvu katika kusimamia weledi wa kazi kwa watumishi wa mahakama nchini.
Profesa Ole Gabriel ameyasema hayo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam na kuongeza kuwa kushika nafasi ya pili kwenye tuzo hizo katika utendaji kazi ni heshima kubwa kwa watendaji wa mahakama hivyo kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii.
Amesema mahakama itaendelea kusimamia mpango mkakati wa kutatua changamoto za wananchi mahakamani kupitia mfumo wa TEHAMA ambao umekuwa msaada mkubwa kwenye utendaji kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa utawala na usimamizi wa rasiliamli watu wa Mahakama ya Tanzania, Beatrice Patrick amesema baadhi ya vigezo vilivyotumika katika utoaji wa tuzo hizo ni nane na kati hivyo ni namna watumishi walivyoweza kutumia mfumo wa kielektroniki kumaliza malalamiko ya wananchi kwa wakati pamoja na mfumo mpya wa kulipa mishahara ya watumishi.
Tuzo hizo zimeandaliwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 kama sehemu ya kutambua mchango wa idara zilizofanya kazi kwa ubora zaidi kwenye masuala ya utawala na usimamizi wa rasilimali watu.