Rais Samia Suluhu Hassan amesema magari 123 yaliyogawiwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) leo na mengine yatakayonunuliwa karibuni ili kufanya jumla ya magari 241 yafungwa mifumo ya kuyafuatilia (car tracking) kujua yalipo, yanafanya nini pamoja na usalama wake.
Rais ametoa agizo hilo mkoani Dar es Salaam katika hafla ya ugawaji wa magari hayo na kuwaonya madereva watakaokabidhiwa kutokuyageuza na kuwa magari ya kubeba abiria au mizigo kama vile magunia ya mkaa, vitendo ambavyo vimekuwa vikitokea mara kwa mara.
Aidha, ameutaka mfuko huo kutojikita tu kwa watu wasio na mali, bali pia uwasaidie hata wenye mali lakini wanaishi maisha duni ili nao waishi maisha mazuri ikiwa ni pamoja na kutoa elimu itakayowakomboa wananchi hao maeneo mbalimbali nchini.
Amewaonya viongozi wenye tabia za kufuja fedha za TASAF akisema kuwa fedha hizo, shilingi trilioni 2, si msaada bali mkopo hivyo zinapaswa kutumika ipasavyo, na wakati wa kulipa unapofika ziwe zimewasaidia Watanzania kutoka kwenye hali duni ya maisha.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF amesema kuwa Tanzania inashika nafasi ya kwanza Afrika na ya pili duniani kwa kujenga uchumi jumuishi.
Ameongeza kuwa mkopo wa shilingi trilioni 2 utatumika katika awamu ya tatu ya kipindi cha pili ambacho kitakamilika mwaka 2025.
Katika mpango huo ruzuku ya shilingi bilioni 200 itatumika kuhudumia kaya zaidi ya milioni moja.