Wahitimu kidato cha sita waitwa mafunzoni JKT

0
142

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetoa wito kwa vijana waliohitimu kidato cha sita kuhudhuria mafunzo ya jeshi hilo kwa mujibu wa sheria.

Wito huo umetolewa mkoani Dar es Salaam na mkuu wa Tawi la Utawala JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena na kufafanua kuwa, vijana wanaotakiwa kujiunga na mafunzo hayo ni wale waliohitimu kidato cha sita mwaka 2022 kutoka shule zote Tanzania Bara.

Brigedia Jenerali Mabena amesema,
vijana walioitwa wamepangwa katika kambi za JKT Rwamkoma Mara, JKT Msange Tabora, JKT Ruvu Pwani, JKT Mpwapwa na Makutupora JKT Dodoma, JKT Mafinga, JKT Mgambo na JKT Maramba Tanga, JKT Makuyuni Arusha, JKT Bulombora, JKT Kanembwa na JKT Mtabila Kigoma, JKT Itaka Songwe, JKT Luwa na JKT Milundikwa Rukwa, JKT Nachingwea Lindi, JKT Kibiti’ Pwani pamoja Oljoro JKT Arusha.

Brigedia Jenerali Mabena pia ameweka wazi kambi ambayo wahitimu wenye Ulemavu wa kuonekana kwa macho wanatakiwa kuripoti ambayo ni Ruvu JKT iliyopo Pwani inayotajwa kuwa na miundombinu rafiki kwa kundi hilo.

Mafunzo hayo ya JKT kwa mujibu wa sheria ni sehemu kwa vijana kujifunza uzalendo, umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha na utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa.