Hukumu ya kesi ya kina Sabaya yaahirishwa

0
151

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha leo imeahirisha hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya na wenzake sita kutokana na Hakimu aliyepangwa kuwa na majukumu mengine.

Imeelezwa mahakamani hapo kuwa shauri hilo lilipangwa kwa ajili ya hukumu hii leo, ila hakimu aliyekuwa akiisikiliza amepangiwa majukumu mengine ya kikazi nje ya ofisi hivyo hukumu itatolewa Juni 10 mwaka huu.

Habari kutoka mkoani Arusha zinaeleza kuwa, mapema hii leo Sabaya na wenzake walifikishwa katika mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi Arusha kwa ajili ya kusikiliza hukumu hiyo.

Hukumu hiyo ambayo kwa sasa imepangwa kutolewa Juni 10 ndio itaamua hatma ya Sabaya na wenzake endapo wataachiwa huru, kwa kuwa mpaka sasa mbali na kesi hiyo hawana kesi nyingine ya kujibu.

Wengine walioshtakiwa na Sabaya katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.