Nchi za Kusini mwa Afrika kuunda mfuko wa kukabiliana na wanyama wakali

0
148

Tanzania imefikia makubaliano na nchi za kusini mwa Afrika kuunda mfuko maalum kwa kila nchi wa kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu hasa tembo.

Hayo yamesemwa na Naibu waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja katika kongamano la Tembo wa Afrika lililofanyika kwenye hifadhi ya Taifa Hwange nchini Zimbabwe.

“Tumekubaliana kwamba kuwepo na mfuko maalum kwa kila nchi ambao utakuwa mahsusi kwa ajili ya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu kama tembo na pia kuwezesha wananchi wanufaike na rasilimali wanyama hao.” amesema Naibu Waziri Masanja

Ameongeza kuwa mfuko huo utakapoanzishwa utawanufaisha wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi na waathirika wa wanyama hao wanaoumizwa au kuuawa kwa kuwezesha kulipwa fidia.

Kongamano hilo la tembo wa Afrika limelenga kuangalia namna jamii zinazoishi pembezoni mwa maeneo ya hifadhi zinavyoweza kushirikishwa katika kutunza rasilimali za wanyama hasa tembo na limehudhuriwa na washiriki kutoka nchi za Tanzania, Botswana, Namibia, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe.