Utafiti kuhusu Uviko-19 kushirikisha hospitali 5 nchini

0
160

Hospitali ya Taifa Muhimbili itaongoza kufanya utafiti wa kuchunguza madhara ya muda mrefu kwa wananchi ambao waliwahi kuugua ugonjwa wa UVIKO-19 (Post Covid Sequelae) kwa ufadhili wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) kupitia Wizara ya Afya.

Utafiti huo wa miezi sita unalenga kubaini madhara ya muda mrefu ambayo huenda yamewapata wananchi waliogua na kupatiwa matibabu ya UVIKO-19 ambapo madhara hayo yanadhaniwa kuathiri baadhi ya viungo vya mwili kama moyo, mapafu, figo, mfumo wa fahamu na viungo vingine.

Akizungumza wakati ya uzinduzi wa utafiti huo, Mtafiti Mkuu, Dkt. Elisha Osati amesema utafiti utashirikisha Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na hospitali tano ambazo ni Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila), Benjamini Mkapa Dodoma, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya (MZRH), Hospitali ya Bugando na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kilimanjaro (KCMC) ambapo zaidi ya sampuli 1,000 zitachunguzwa.

“Mbali na kuchunguza madhara ambayo huenda viungo ambavyo nimevitaja wameyapata lakini pia utafiti umelenga kubaini hali za kiuchumi za wananchi hao ikiwemo gharama halisi walizotumia kupata matibabu,” amesema Dkt. Osati.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa utafiti huo, amesema ni wakati sasa kwa wataalamu wazalendo kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitaleta majawabu chanya kwenye jamii.

“Wakati dunia ilipoingia kwenye tatizo la UVIKO-19 kulikuwa na tafiti mbalimbali ambazo zimefanywa duniani, lakini ni asilimia tatu tu ndizo zilifanywa na Waafrika ambazo sana sana zilitokea Afrika ya Kusini, Misri na Nigeria” amesema Prof. Museru.

Amesema hakukuwa na utafiti rasmi uliofanywa wa wataalamu wazalendo kuhusu tiba mbalimbali zilizotumika wakati huo ikiwemo tiba mbadala ya kujifukiza (Steam Therapy) na kwamba huu ni wakati sasa wa dunia kusikia matokeo ya tafiti kutoka Afrika.