Dkt. Mpango: Tafiti zisaidie Afrika wakati wa majanga

0
109

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango leo tarehe 25 Mei 2022 ameshiriki katika majadiliano maalum ya viongozi wakuu wa nchi za Afrika katika ajenda iliohusu namna Bara la Afrika linavyoweza kubadili utaratibu wa kimataifa katika kukabiliana na masuala mbalimbali, majadiliano yaliofanyika katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani unaoendelea Davos nchini Uswisi.

Akizungumza katika majadiliano hayo, Makamu wa Rais amesema ni muhimu nchi za Afrika kushirikiana katika kuwezesha tafiti za ndani ya nchi ili kukabiliana na majanga mbalimbali yanapojitokeza pasipo utegemezi.

Makamu wa Rais ameitaja taasisi ya Taifa ya utafiti ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR) iliopo nchini Tanzania pamoja na taasisi zingine za ndani ya nchi zilitoa msaada mkubwa wakati wa kukabiliana na Uviko 19.

Amesema ni muhimu kushirikiana na sekta binafsi zilizopo ndani ya nchi kwani zimekua zikitoa mchango mkubwa hasa wakati wa kukabiliana na majanga mbalimbali.

Aidha Makamu wa Rais amesema kwa kutumia rasilimali zilizopo, mataifa ya Afrika yanaweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza na kuongeza kwamba kwa sasa Tanzania inazalisha chanjo ya mifugo hivyo hakuna budi mataifa ya Afrika kuungana katika uzalishaji huo utakaosaidia mahitaji ya baadae.

Mkutano huo umeshirikisha viongozi wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika pamoja na wawakilishi kutoka mataifa hayo.