Tanzania haina Monkeypox

0
118

Wizara ya Afya imesema Tanzania haina mgonjwa wa “Monkeypox” aliyewahi kugundulika.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu ugonjwa huo.

Amewataka wananchi wote kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na kuzuia magonjwa ya kuambukizwa na yale ya mlipuko ikiwa ni pamoja na usafi binafsi na usafi wa mazingira.

Dkt. Molllel pia amewataka wananchi kutogusa, kula mnyama anaeumwa au mzoga au kugusa vitu vilivyotumika na mnyama mgonjwa au mzoga.

Na kwa nyama ameshauri ipikwe na iive vizuri.

Tarehe 16 mwezi huu Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa taarifa ya kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa “Monkeypox” nchini Uingereza.

Mpaka tarehe 20 mwezi huu watu 38 walikuwa wamekwisha thibitika kuwa na ugonjwa huo kutoka nchi mbalimbali duniani ambazo ni Uingereza, Ubelgiji, Ufaransa, Italia, Ureno, Hispania, Uswisi, Canada na Marekani.

“Monkeypox” ni ugonjwa unaotokea mara nyingi kwenye nchi za Afrika ya kati na Afrika ya Magharibi kwenye misitu ya mvua za kitropiki ambapo wanyama jamii ya nyani, panya na kindi wenye virusi hivyo ndipo wanapoishi.

Monkeypox ni ugonjwa unaoweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama wenye maambukizi kwenda kwa binadamu na kutoka kwa binadamu kwenda
kwa binadamu endapo mtu asiye na maambukizi atagusana na mtu mwenye maambukizi kipindi anapokuwa na dalili.

Virusi vinaweza kuingia mwilini kupitia ngozi iliyo na jeraha au michubuko, kwa njia ya upumuaji (hewa) au kupitia macho, pua au mdomo.

Unaweza pia kuenezwa kwa kugusa vitu kama vile matandiko na nguo alizotumia mgonjwa.

Dalili kuu za ugonjwa huo ni pamoja na homa, vipele vinavyoweza kuwa na majimaji au usaha hasa sehemu za uso, viganja vya mikono na nyayo za miguu, mwili kuchoka na kichwa kuuma.

Dalili za ugonjwa hudumu kati ya wiki mbili mpaka nne na kwa kawaida ugonjwa huwa si mkali na wakati mwingine hufanana na tetekuwanga na hupona bila dawa.

Aidha, mara chache ugonjwa unaweza kuwa mkali zaidi na kupelekea kifo hasa kwa watoto wachanga na watu wenye magonjwa yanayodhoofisha kinga ya mwili.