Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amefanya kikao na wakandarasi wanaojenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano jijini Dodoma ambapo amesema kuwa Wizara anayoisimamia ipo tayari kujenga uchumi wa kidijitali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaamini katika ushirikiano na Sekta Binafsi katika kuendesha shughuli zake kwa kuwa ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.
“Inawezekana hapa na pale Sekta Binafsi imekutana na mawimbi mbalimbali lakini tunawahakikishia kuwa mawimbi yametulia na tupo tayari kufanya kazi pamoja na tuwahakikishie kuwa tutawalinda ili mradi mtimize wajibu wenu na mfanye kazi kwa kuzingatia muda, viwango na ubora wa kimataifa”, amesema Waziri Nape.
Waziri Nape amesema kuwa wakandarasi wazawa wanafanya vizuri na ni matamanio ya Serikali kuwa idadi yao izidi kuongezeka ambapo amesema kwa mwaka wa fedha unaomalizika Juni 30, 2022 jumla ya Mikataba 22 ya ujenzi wa kilomita 4,442 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano imeingiwa baina ya Wizara na Wakandarasi 8 ambao kati yao wakandarasi 6 ni wazawa na wakandarasi 2 wanatoka katika kampuni za nje zilizosajiliwa nchini
Kwa upande wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limepewa cheti kwa kumaliza ujenzi wa Kilomita 72 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano uliojengwa kuunganisha ofisi za Serikali Dodoma.