Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeunga mkono na kuridhia hatua ya Mwenyekiti wa chama hicho Rais Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza majadiliano na vyama vya siasa yenye lengo la kuimarisha demokrasia kupitia maridhiano ya kisiasa kwa maslahi ya Taifa.
Katibu wa halmashauri kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka amesema CCM inasisitiza kuendeleza majadiliano hayo kwa dhumuni la kujenga jamii yenye usawa, uhuru wa kujieleza na kushiriki shughuli za kisiasa kwa kuzingatia maadili na sheria za nchi.
Akizungumzia kikao Kamati Kuu ya CCM kilichofanyika hivi karibuni jijini Dodoma kwa ajili ya kupokea kisha kujadili masuala mbalimbali ya kitaifa, Shaka amesema
“Kamati kuu ilipokea na kujadili masuala ya mbalimbali ya kitaifa ikiwemo hatua zinazochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kujenga maridhiano ya kisiasa nchini. Kamati Kuu imempongeza na kumuunga mkono Rais Samia kwa hatua anazoendelea kuchukua ikiwemo kukutana na kufanya mazungumzo na makundi ya kijamii katika kujenga amani, haki na maridhiano.”
Shaka amesema Kamati Kuu ya CCM imetambua na kuridhia dhamira ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufanya maridhiano kwa kuzingatia uendelezaji wa urithi, tunu na msingi imara wa ujenzi wa Taifa ili kuviwezesha vizazi vijavyo virithi Taifa jema na lililo imara.